Takriban mashabiki 11,400 wameongezwa kuhudhuria robo fainali ya kombe la CHAN baina ya Kenya na Madagascar leo Ijumaa katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.
Waziri wa Michezo Salim Mvurya ametangaza kuwa Shirikisho la Soka Afrika, CAF limekubali kuongeza idadi ya mashabiki kutoka asilimia 60, sawa na 27,000, hadi asilimia 80, sawa na 38,400, kwa mechi hiyo.
Awali, CAF ilipunguza idadi hiyo hadi 27,000 katika mchuano wa kundi A kati ya Kenya na Zambia kutoka 48,000, baada ya mashabiki kukiuka sheria wakati wa mechi baina ya Kenya na Morocco.
Pambano hilo litapigwa kuanzia saa kumi na moja jioni.