Mwanamuziki nguli wa Uganda Joseph Mayanja maarufu kama Jose Chameleone anaripotiwa hatimaye kukubali kuhitimisha ndoa yake na Daniella Atim.
Wawili hao walioana Juni 7, 2008.
Atim ambaye anaishi nchini Marekani na ambaye ana watoto na Chameleone aliwasilisha ombi la talaka mwezi Machi mwaka huu.
Katika ombi lake la talaka mahakamani, Daniella alitaja sababu kadhaa za kutaka kuachana na Chameleone zinazojumuisha kutelekezwa, kutopendwa na kutosaidiwa.
Kulingana naye, Chameleone amemtelekeza kwa miaka mitano hali iliyomlazimisha ajitunze pamoja na watoto wao.
Atim anadai usimamizi kamili wa watoto, umiliki wa makazi yao ya Seguku huko Makindye jijini Kampala nchini Uganda na usaidizi endelevu kutoka kwa Chameleone kwake na kwa wanao.
Anataka Chameleone pia alipe gharama ya kesi hiyo.
Kwa upande wake Chameleone anataka makazi hayo ya Seguku yasalie kuwa mali ya familia na anataka aruhusiwe pia kuendelea kuwa kwenye maisha ya wanawe.
Chameleone ambaye anaendelea kupona ugonjwa wa kongosho uliosababisha aende Marekani kutibiwa, anasema kwamba Atim amefanya wanao wasimpende kama baba.
Kuhusu kuendelea kugharamia maisha ya Atim na watoto, Chameleone anaamini kwamba wazazi wote wawili wanastahili kuchangia kwani wote wanafanya kazi.
Alikanusha madai ya Atim kwamba alitelekeza mkewe na watoto akifafanua kwamba walikubaliana kuhamishia wanao Marekani mwaka 2018.
Jose Chameleone anasema yeye ndiye alinunua nyumba ambayo Atim na watoto wanaishi na amekuwa akiwapa usaidizi inavyostahili.