Jaji Frank Caprio afariki

Haya yanajiri yapata miaka miwili tangu alipotangaza kwamba amegunduliwa kuwa na maradhi ya saratani.

Marion Bosire
2 Min Read

Familia ya Jaji maarufu wa Marekani Frank Caprio imetangaza kifo chake kilichotokea akiwa na umri wa miaka 88.

Kulingana na tangazo kwenye akaunti yake rasmi ya Instagram, kifo cha Caprio kinaaminika kusababishwa na ugonjwa wa saratani ya kongosho aliogunduliwa kuwa nao.

Jaji Caprio alijipatia umaarufu ulimwenguni kutokana na maamuzi ya kesi mbali mbali ambapo alidhihirisha utu na wema bila kusahau vichekesho.

Video za kazi zake katika kipindi “Caught in Providence” zilisambaa mitandaoni na kugusa watu wengi katika sehemu mbali mbali ambao mara nyingi walitoa michango ya kifedha kusaidia wateja wake.

Caprio alitekeleza kazi yake kwa muda wa miaka kama arobaini katika mji wa Providence, eneo la Rhode Island, wema wake ukisababisha arejelewe kama Jaji mwema kabisa ulimwenguni kote.

Kampuni inayodhamini kipindi chake kwa jina Debmar-Mercury imetoa ujumbe wa kumwomboleza Caprio ikimtaja kuwa nembo ya kipekee ya kutatua kesi kwa njia ya utu na wa fikra thabiti.

Katika taarifa wasimamizi wawili wakuu wa kampuni hiyo Mort Marcus na Ira Bernstein walisema watamkosa sana Caprio.

Baada ya kugunduliwa kuwa na saratani ya kongosho mwaka 2023, Jaji Caprio alionyesha ujasiri ambapo alisema kwamba alikuwa tayari kupambana na maradhi hayo kwa uwezo wake wote.

Alishukuru wafuasi wake mitandaoni kwa kumsaidia huku akiwafahamisha kila mara kuhusu kuugua kwake na kuwataka wamwombee.

Jaji Caprio ameacha mke wake waliyekuwa naye kwenye ndoa kwa miaka kama 60 Joyce Caprio, wanao watano, wajukuu saba na vitukuu wawili.

Share This Article