Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua amerejea nchini kutoka Marekani.
Gachagua aliwasili nchini majira ya saa saba mchana na kulakiwa na wafuasi wake waliomsubiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA.
Gachagua, aliyeandamana na mkewe, Dorcas Rigathi, amekuwa nchini Marekani kwa kipindi cha wiki sita zilizopita.
Wakati wa ziara yake nchini humo, Naibu Rais huyo wa zamani alikutana na Wakenya wanaoishi nchini humo na kutumia fursa hiyo kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza aliyoitumikia wakati mmoja.
Ripoti zinaashiria alikatiza ziara yake Marekani na kurejea nchini kuongoza kampeni za chama chake cha DCP katika chaguzi ndogo mbalimbali zilizopangwa kufanyika Novemba 27, ikiwa ni pamoja na uchaguzi mdogo wa Malava.