Kenya imesaini makubaliano kadhaa ya ushirikiano wa kimaendeleo na Japani katika Kongamano la Kimataifa la Tokyo kuhusu Maendeleo barani Afrika, TICAD, mjini Yokohama, nchini Japani.
Makubaliano hayo ni pamoja na taarifa ya dhihirisho la utashi kuhusu hati ya Samura (Samurai Bondo), kibali cha kifedha kinachotolewa kwa mataifa ya kigeni katika masoko ya mtaji nchini Japani kilichosainiwa kati ya Hazina Kuu ya Kenya na kampuni ya kuuza bidhaa nje ya nchi na bima za uwekezaji – Nippon.
Aidha, serikali ya Kenya ilisaini dhihirisho la utashi la kuongeza upatikanaji haraka wa dawa ya Cefiderocol inayotumika kutibu homa ya mapafu nchini Kenya.
Mwafaka huo ulisainiwa kati ya Wizara ya Afya ya Kenya na kampuni ya Shionogi ya Japani, inayohusika na utafiti wa kimatibabu.
Pia Kenya ilisaini ushirikiano wa maendeleo ya nguvukazi kati ya taasisi ya utafiti wa kiviwandani nchini na Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda nchini Japani.