Wimbo wa 2Baba African Queen watambuliwa na Billboard

Jarida la Billboard lilichapisha orodha ya nyimbo 50 bora za mtindo wa Afrobeats ambapo African Queen uliibuka kidedea.

Marion Bosire
2 Min Read

Jarida maarufu la muziki nchini Marekani Billboard limetambua wimbo wa zamani wa mwanamuziki wa muda mrefu wa Nigeria Innocent Idibia maarufu kama 2Baba uitwao African Queen.

Billboard ilichapisha orodha ya nyimbo 50 bora za mtindo wa Afrobeats ambapo African Queen uliozinduliwa mwaka 2004, ulichukua nafasi ya kwanza na kushinda hata miziki ya hivi punde zaidi ya mtindo huo.

Wimbo wa Wizkid Ojuelegba uliorodheshwa nambari mbili, Nwa Baby wa Favour nambari 3, Calm Down wa Rema nambari 4 huku Wizkid akirejea tena katika nafasi ya tano na wimbo wake Essence alioshirikisha Tems.

Wimbo ulioimbwa na CKay uitwao Love Nwantiti, wa D’banj Oliver Twist, wa Davido Fall, wa Burna Boy Ye na wa P-Square Chop My Money Remix zinakamilisha orodha ya 10 bora kulingana na Billboard.

Nyimbo za wasanii wa Nigeria zilitawala nafasi za kwanza 20 za orodha hiyo lakini wasanii wa Ghana pia walijipatia nafasi humo ambapo nyimbo za Azonto na Adonai ziliorodheshwa nambari 18 na 19 mtawalia.

Yemi Alade ndiye msanii wa kike aliyeongoza kwenye orodha hiyo ambapo wimbo wake Johnny uko nambari 15. Wengine ni Wande Coal ambaye wimbo wake Bumper to Bumper umeorodheshwa nambari 17 na Fada Fada ulioimbwa na Phyno akimshirikisha Olamide uko nambari 20.

Mtindo wa Afrobeats unaohusishwa na wasanii wa nchi za Magharibi ya Afrika umejipatia umaarufu katika miaka ya hivi karibuni ulimwenguni kiasi cha kujumuishwa kwenye tuzo za hadhi ya juu zaidi za Grammy.

Share This Article