Mwanamuziki wa Marekani Offset amesema kwamba amekubali kwamba uhusiano kati yake na mama ya watoto wake Cardi B umetamatika akisema ulikuwa mzuri ulipokuwepo.
Msanii huyo alikuwa akizungumza kwenye mahojiano na jarida moja maarufu la Marekani ambapo alisisitiza kwamba suala hilo halifai hata kuzungumziwa tena.
Mahojiano hayo yalilenga kuangazia albamu yake ijayo kwa jina “KIARI” ambalo ni jina lake ambapo alisema kwamba wimbo wa mwisho kwenye Albamu hiyo unazungumzia uhusiano huo ulioharibika.
“Ilipofikia sasa ni kila mmoja kuendelea na maisha yake kwa amani. Huo ndio unastahili kuwa ujumbe.” Alisema msanii huyo.
Aliendelea kuelezea kwamba kilichosalia zaza ni mapenzi na amani ndiposa aliamua kumalizia albamu yake na suala hilo kama njia ya kufunga sura hiyo kabisa.
Cardi aliwasilisha ombi la talaka Agosti 2024, Februari mwaka huu Offset akaomba mahakama iwape haki sawa za kulea wanao watatu lakini makazi yao rasmi yawe jumba la Cardi B.
Mwezi Mei iliripotiwa kwamba Offset alikuwa amebadili maombi yake kwa mahakama na kuongeza lile la kutaka awe akipata pesa za kujikimu kutoka kwa Cardi.
Cardi alipinga vikali ombi hilo mitandaoni kiasi cha kufichua kwamba alikuwa anagharamikia watoto wao watatu kikamilifu bila usaidizi wa Offset ambaye ni mzazi mwenza.
Alifafanua kwamba Offset yuko huru kutembelea watoto wao na kuwajulia hali kinyume na madai yake kwamba amewekewa vikwazo, akiongeza kwamba Offset ameona mwanao mdogo aliyezaliwa Septemba 2024 mara tano pekee.
Wawili hao hata hivyo wataendelea kuonana maishani kwani wanatarajiwa kushirikiana kutunza watoto hao Kulture Kiari aliye na umri wa miaka 7, Wave Set wa miaka mitatu na Blossom wa miezi 11.