Bunge la Kitaifa litasitisha vikao vyake kesho Jumatano Agosti 20, ili kuwaruhusu wabunge kuchukua likizo fupi ya mwezi mmoja hadi Septemba 22.
Wabunge kwa kauli moja wamepitishwa hoja iliyoowasilishwa bungeni na kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah leo Jumanne alasiri.
Likizo hiyo itaanza kesho Jumatano Agosti 20 na kukamilika Jumatatu, Septemba 22, 2025.
Kisha bunge litarejelea vikao vyake Septemba 23.
Wabunge wanaelekea likizoni wakati mawingu ya madai ya kukithiri kwa ufisadi katika kamati za bunge yametanda kotekote.
Rais William Ruto amezituhumu kamati hizo kwa kuwa na hulka ya kuitisha hongo kutoka kwa watu wanaofika mbele yake kuwajibishwa.
Ni madai ambayo wabunge wamekanusha vikali wakiutaka uongozi wa nchi kuyathibitisha kwa kuwataja wahusika.
Kwa upande wake, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC, imeapa kuyachunguza madai hayo na kuwawajibisha wahusika ikiwa yatabainishwa.