Seneti kujadili kubanduliwa kwa Gavana wa Kericho kesho

Afisi ya spika wa Seneti ilifahamishwa kuhusu kuondolewa madarakani kwa Gavana Eric Mutai Agosti 15, 2025.

Marion Bosire
2 Min Read
Gavana wa Kericho Erick Mutai

Bunge la Seneti litaandaa kikao maalum kesho Jumatano Agosti 20, 2025 kujadili hoja ya kubanduliwa madarakani kwa gavana wa kaunti ya Kericho Eric Kipkoech Mutai na bunge la kaunti ya Kericho.

Kulingana na chapisho kwenye gazeti rasmi la serikali la Agosti 18, 2025, Spika wa Seneti Amason Jeffah Kingi ameitisha kikao kulingana na sehemu ya 33 ya kanuni za Seneti.

Hatua yake inajiri kufuatia barua aliyopokea kutoka kwa spika wa bunge la kaunti ya Kericho Agosti 15, 2025, iliyomfahamisha kuhusu uamuzi wa bunge hilo wa kumg’atua mamlakani Gavana Mutai.

Kikao hicho kitaanza saa nane unusu alasiri na kando na suala hilo, kitatoa fursa ya kuapishwa kwa Seneta mteule Consolata Nabwire Wakwabubi na mabadiliko ya kalenda ya Seneti.

Wakwabubi ameteuliwa chini ya kifungu nambari 98 sehemu ya kwanza (b) cha katiba ya Kenya kuwakilisha wanawake katika bunge la Seneti ambapo anachukua mahala pa Gloria Orwoba.

Gavana Mutai ndiye Gavana wa hivi punde zaidi kukabiliwa na uwezekano wa kuondolewa mamlakani baada ya jaribio la kumbandua Gavana wa Isiolo Abdi Guyo kugonga mwamba.

Mutai tayari amepinga hatua hiyo akidai kwamba ana ushahidi unaoonyesha kwamba shughuli ya kupigia kura hoja ya kumbandua madarakani katika bunge la kaunti ya Kericho ilikumbwa na dosari.

Hii ni mara ya pili Gavana Mutai anakumbwa na tatizo hili. Aliwahi kubanduliwa na wawakilishi wadi wa Kericho Oktoba 2024     ambapo maseneta 34 walipiga kura ya kukubaliana na mawakili wake huku 10 wakiunga mkono uamuzi wa bunge la kaunti ya Kericho.

Share This Article