Waziri wa Afya Aden Duale amefanya mabadiliko katika usimamizi wa hospitali kuu ya Kenyatta, KNH ambapo amemteua Dkt. Richard Lesiyampe Leserian kuwa kaimu afisa mkuu mtendaji.
Katika taarifa aliyotoa jana, Agosti 18, 2025, Duale alielezea kwamba serikali imetambua utoaji wa huduma za afya kuwa nguzo kuu ya ajenda ya uwezeshaji ya “Bottom-Up”.
Alitaja pia hospitali ya kitaifa ya Kenyatta kuwa taasisi kuu ya rufaa aliyosema ni muhimu katika kuendeleza mabadiliko ya sekta ya afya na kuafikia mpango wa huduma bora za afya kwa wote, UHC.
“Ili kupiga jeki wajibu huu, Dakta Richard Lesiyampe Leserian amehamishwa kuwa kaimu afisa mkuu mtendaji wa hospitali ya kitaifa ya Kenyatta” alisema Waziri katika taarifa yake.
Alimsifia Lesiyampe ambaye amekuwa akihudumu kama afisa mkuu mtendaji wa hospitali ya mafunzo na rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga akisema ana tajriba kuu itakayoimarisha usimamizi wa hospitali ya kitaifa ya Kenyatta.
Kando na usimamizi, Duale alisema pia kwamba Lesiyampe atapiga jeki mifumo ya utoaji huduma za afya na ya usimamizi katika taasisi hiyo ya kitaifa ya afya.
Waziri Duale alitangaza pia uteuzi wa Joshua Clinton Ombiri Okise kuwa kaimu afisa mkuu mtendaji wa hospitali ya mafunzo na rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga kujaza nafasi iliyoachwa na Lesiyampe.
Okise amejukumiwa kuhakikisha ubadilishanaji laini wa uongozi katika taasisi hiyo ya Kisumu na kusaidia kuendeleza ukuaji wake kufuatia kupandishwa hadhi kwa hospitali hiyo hivi maajuzi hadi kiwango cha Level 6.