Gavana wa Kericho Erick Mutai alibanduliwa jana jioni katika kikao kilichochukua zaidi ya saa 10 katika bunge la Kaunti ya Kericho.
Jumla ya wawakilishi wadi 33 walipiga kura kuunga mkono hoja hiyo, huku 14 wakiipinga kupitia mfumo wa kielektroniki.
Punde tu baada ya Spika wa Bunge hilo Patrick Mutai kutangaza matokeo hayo, mzozo uliibuka baina ya wawakilishi wadi hao, huku baadhi yao wakipinga matokeo hayo.
Wawakilishi wadi wanaomuunga mkono Gavana huyo, walipinga upigaji kura kutumia mfumo wa kielektroniki, wakisema kulikuwa na wizi wa kura ili kufanikisha kumtimua Gavana huyo.
Gavana huyo aliondolewa mamlakani kwa madai ya ukiukaji wa katiba, utumizi mbaya wa mamlaka na ukosefu wa maadili.
Anadaiwa kufanikisha ulipaji wa shilingi milioni 85 kwa wanakandarasi na wasambazaji bidhaa kinyume cha sheria.
Awali Gavana huyo alikuwa ametetewa na wakili wake mkuu Katwa Kigen, aliyewasihi wawakilishi wadi hao kumuokoa kutokana na tuhuma dhidi yake.