Shirika la AMREF Flying Doctors, limerejelea shughuli zake wiki moja baada ya moja ya ndege zake kuanguka katika eneo la Mwihoko kaunti ya Kiambu,ambapo wafanyakazi wake wanne walifariki.
Akizungumza na wanahabari katika afisi za shirika hilo kwenye uwanja wa ndege wa Wilson, Afisa Mkuu Mtendaji wa AMREF Dkt. Githinji Gitahi, alithibitisha kuwa shughuli ya kwanza baada ya ajali hiyo, ilihusisha safari ya ndege yake kutoka Nairobi kuelekea Belgium kumsaidia mwathiriwa wa ajali.
Dkt. Githinji alidokeza kuwa AMREF inaendelea kutoa ushauri nasaha kwa familia za waathiriwa wa ajali ya Mwihoko, huku mipango ya mazishi ya walioagamia kwenye ajali hiyo ikitarajiwa kuanza wiki ijayo.

Ndege hiyo ya AMREF aina ya Cessna Citation 560XL, iliyoanguka, ilikuwa ikielekea Hargeisa, katika jimbo la Somaliland, lilipopoteza mawasiliano na maafisa wa kuongoza safari za ndege muda mfupi baada ya kuondoka katika uwanja wa ndge.
Ndege hiyo ilianguka katika nyumba ya makazi, na kuwaua watu sita na kuwajeruhi wawili.
Miongoni mwa waliofariki ni pamoja na Madaktari wawili, Wauguzi wawili na raia wawili waliokuwa mahala pa ajali.
Halmashauri ya safari za ndege KCAA, inaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.