Kuimarisha uzalishaji wa viazi Nyandarua kupitia teknolojia ya miche ya Apical

Martin Mwanje
5 Min Read

Baraza la Kitaifa la Viazi nchini Kenya (NPCK) limeongeza juhudi za kuandaa, kupanga na kuratibu mnyororo wa thamani wa viazi kwa wakulima wadogo katika Kaunti ya Nyandarua, kwa kulenga sana utumiaji wa teknolojia ya kisasa ya mbegu ili kuongeza uzalishaji.

Mojawapo ya miradi ya hivi karibuni ni shamba la mfano lililoanzishwa na kikundi cha Blessed Unit Self Help Group katika kijiji cha Memo, wadi ya Murungaru, eneobunge la Kinangop. Shamba hili linatumia teknolojia mpya ya miche ya viazi inayojulikana kama Apical Rooted Cuttings (ARCs), ambayo ilianzishwa miezi mitatu iliyopita na tayari imeonyesha mafanikio makubwa ikilinganishwa na mbegu za kawaida za “mini-tubers”.

Kwa mujibu wa Henry Chemjor kutoka NPCK, teknolojia ya mbegu ya Apical inaharakisha uzalishaji wa mbegu na kuwezesha wakulima wadogo kupata mbegu bora kwa haraka. “Miche hii ina ubora sawa na mbegu ya kiwango cha awali (pre-basic seed). Tofauti na njia za kawaida kama vile kutumia mini tubers au teknolojia ya aeroponics, miche hii huwezesha uzalishaji wa haraka wa mbegu nyingi,” alisema Chamjor.

Aliongeza kuwa kutoka kwa miche hii, wakulima wanaweza kuzalisha mbegu katika hatua mbalimbali—C1, C2 na C3—na hatimaye kuwa na mbegu za kutosha kwa matumizi ya kibiashara. Hata hivyo, Chamjor alitaja kuwa changamoto kubwa bado ni upatikanaji wa mbegu bora, kwani ni ghali na haipatikani kwa urahisi. Hali hii inawalazimu wakulima wengi kutumia mbegu zilizorejelewa (recycled), ambazo mara nyingi huwa na ubora hafifu na kusababisha mavuno duni.

Kupitia aina za viazi kama Wanjiku, Unica na Shangi kwa kutumia teknolojia ya Apical, wakulima wanaanza kupata mbegu safi na bora kwa urahisi zaidi. Matumizi ya mbegu safi ni muhimu sana katika kilimo cha viazi kwani huongeza kiwango cha uotaji, hupunguza magonjwa, na kuongeza mavuno. Pia hupunguza utegemezi wa kemikali nyingi, na kutoa mazao bora yanayokubalika sokoni.

Mradi huu pia unapata msaada kutoka kwa Shirika la ASARECA (Association for Strengthening Agricultural Research in Eastern and Central Africa). Afisa wa Ufuatiliaji na Tathmini wa shirika hilo, Moses Odeke, alisema kuwa mradi huu unalenga kuhamasisha wakulima kuhusu teknolojia mpya na kuinua maisha ya wakulima wadogo. Alifichua kuwa mradi wa Blessed Unit Self Help Group unafadhiliwa pia na Umoja wa Ulaya (EU) na unasimamiwa na shirika la IFAD.

“Teknolojia ya miche ya Apical inazalisha mbegu nyingi zenye uwezo mkubwa wa kustahimili magonjwa na zinazohitajika sana sokoni,” alisema Odeke. “Tulichagua Nyandarua kwa sababu wakulima hapa wana ari kubwa ya kupanda aina mpya za viazi, jambo lililowapa ASARECA fursa ya kuingia katika eneo hili.”


Kuhusu mjadala unaoendelea kuhusu matumizi ya dawa hatari kwenye viazi, Odeke alihimiza wakulima kutumia tu viuatilifu vilivyopendekezwa na kwa viwango vinavyofaa, pamoja na kuhusisha maafisa wa ugani kwa ushauri wa kitaalamu.

Serikali ya Kaunti ya Nyandarua pia imejitolea kikamilifu kuunga mkono mradi huu. Afisa Mkuu wa Idara ya Kilimo, Kamau Gitaka, alisema kuwa chini ya uongozi wa Gavana Kiarie Moses Badilisha, kaunti imeanzisha Kitengo cha Uzalishaji wa Viazi katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo (ATC) kilichopo Ol Joro Orok, ambako kuna maabara ya tissue culture ya kuzalisha miche ya Apical.

“Kikundi hiki cha Blessed Unit tunakiunga mkono kwa asilimia mia moja ili kuinua maisha ya wakulima wa wadi ya Murungaru,” alisema Gitaka. “Kila msimu wa kupanda huongeza idadi ya miche, hivyo basi kuhakikisha kuna mbegu za kutosha kwa wakulima.”

Rebecca Kuria, mmoja wa wanachama wa kikundi cha Blessed Unit, alieleza matumaini makubwa juu ya mafanikio ya teknolojia hii. “Mavuno kutoka kwa shamba letu la majaribio yamekuwa ya kuvutia sana. Aina ya Wanjiku ilizalisha kati ya mbegu 20 hadi 60 kwa kila mmea, Shangi 15 hadi 30, na Unica kati ya 12 hadi 30,” alisema.

Kwa teknolojia kama hii ya miche ya Apical, mustakabali wa kilimo cha viazi katika Kaunti ya Nyandarua unaonekana kuwa na matumaini makubwa, huku wakulima wakifurahia mavuno bora, mbegu safi na maisha bora zaidi.

Share This Article