Wenyeji wenza wa fainali za kombe la CHAN, Harambee Stars ya Kenya, walijikatia tiketi kwa hatua ya robo fainali jana usiku baada ya DR Congo kuwanyuka Angola magoli mawili kwa nunge katika kundi A.
Kenya watashuka uwanjani Kasarani Jumapili kwa mechi dhidi ya Zambia, kuhitimisha hatua ya makundi wakiwa tayari wamefuzu kwa hatua ya nane bora.
Stars watakuwa wakilenga kuongoza kundi hilo ili kucheza robo fainali uwanjani Kasarani.
Mabingwa mara mbili Morocco wametoshana na DRC kwa alama sita kila moja baada ya kuwazabua Zambia 3-1, jana jioni.
Kenya ina alama 7, ikifuatwa na Morocco na DRC kwa pointi 6, huku Angola ikiwa na alama 4.
Harambee Stars wanajiunga na Taifa Stars kutoka Tanzania, ambao ni wenyeji wenza wa kipute hicho katika hatua ya kwota fainali.