Kaunti ya Nyandarua imetikiswa na matukio mawili ya kusikitisha ambapo msichana wa umri wa miaka 13 alibakwa na kuuawa kijijini Mugumo, Olkalou.
Kwenye tukio lingine, askofu mashuhuri wa Akorino alifariki dunia baada ya jengo la kanisa lake kuporomoka akiwa ndani pamoja na wanawe wawili huko Heni, Kinangop.
Kwenye tukio la kwanza katika kijiji cha Mugumo, familia moja imejipata katika majonzi makubwa baada ya kumpoteza Maureen Wanjiku, mwanafunzi wa Darasa la Saba katika Shule ya Msingi ya Mugumo. Maureen alitumwa dukani kununua sukari Jumanne alasiri lakini hakurudi nyumbani.
Kulingana na babu yake, James Thiong’o, alikuwa ameenda kumtembelea mama ya Maureen katika Hospitali ya JM Memorial, ambako alikuwa amejifungua pacha. Aliporejea nyumbani, aliambiwa kuwa Maureen hakuwa amerudi.
Harakati za kumtafuta zilianza mara moja na zikaendelea hadi usiku wa manane.
Asubuhi iliyofuata, juhudi hizo ziliendelea zikiongozwa na mjomba wake Peter Thiong’o na babu na nyanya yake. Kwa masikitiko makubwa, waligundua mwili wa Maureen ukiwa umetupwa chini ya shamba lao.
Kamanda wa Polisi wa kaunti ya Nyandarua, Stella Cherono, alithibitisha kwamba msichana huyo alibakwa kabla ya kuuawa.
“Tumeanzisha uchunguzi kamili na tunafuatilia kila taarifa ili kuhakikisha mhusika anapatikana na kufikishwa mahakamani,” alisema.
Familia hiyo imetoa wito wa haki kutendeka haraka na kuhakikisha kuwa aliyehusika anakamatwa. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya JM Memorial ukisubiri kufanyiwa upasuaji.
Katika tukio tofauti lililotokea katika kijiji cha Heni, wadi ya Githabai, tarafa ya Kinangop, jamii inalia kwa huzuni kufuatia kifo cha ghafla cha Askofu Hirum Kibue wa Kanisa la Holy Mission Israel baada ya jengo la kanisa hilo kuporomoka akiwa ndani pamoja na wanawe wawili.

Kwa mujibu wa Askofu Zachary Njoroge wa Kanisa la Calvary lililo jirani, Askofu Kibue na wanawe walikuwa wakiondoa mbao za kuunganisha zege katika ujenzi wa ghorofa mpya ya kanisa hilo, walipokumbwa na mkasa huo.
Askofu Kibue alifariki papo hapo huku wanawe wakijeruhiwa vibaya.
Wanawe walipelekwa katika Kituo cha Afya cha Heni kwa matibabu, huku mwili wa Askofu Kibue ukipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Engineer.
Matukio hayo mawili yamesababisha simanzi kubwa miongoni mwa wakazi wa Nyandarua, ambapo viongozi wa kaunti na jamii kwa ujumla wanatoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina, kuwekwa kwa hatua madhubuti za usalama kwenye maeneo ya ujenzi, na ulinzi zaidi kwa watoto na familia.
Wakati uchunguzi ukiendelea, familia zimo katika majonzi makubwa, zikiomba haki, faraja, na majibu kufuatia mikasa hiyo miwili ya kusikitisha.