Ruto asifia ugatuzi, asema umechochea maendeleo makubwa nchini

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto ameulimbikizia sifa mfumo wa ugatuzi akisema umechochea maendeleo makubwa katika kila pembe ya nchi.

Ruto ameahidi kuhakikisha majukumu yaliyosalia yanakabidhiwa serikali za kaunti katika hatua anayosema itasaidia kuboresha utoaji huduma kwa raia.

Wakati huo huo, ameahidi kuwa serikali imekusudia kutoa rasilimali zaidi zinazohitajika kuchochea maendeleo nchini.

Ametoa mfano wa fedha za mwezi Julai mwaka huu ambazo tayari serikali kuu imezitoa kwa serikali za kaunti ili kuhakikisha zinatekeleza majukumu yake ipasavyo.

Akizungumza wakati akifungua rasmi Kongamano la Ugatuzi 2025, Rais Ruto amesema hadi kufikia sasa, jumla ya shilingi trilioni 4 zimetolewa kwa serikali za kaunti tangu kuasisiwa kwa mfumo wa ugatuzi miaka 13 iliyopita.

Kadhalika, alirejelea Mswada wa Kaunti wa Ugavi wa Mapato alioutia saini kuwa sheria leo Jumatano akisema utahakikisha serikali za kaunti zinapata shilingi bilioni 30 zaidi ili kuboresha huduma zinazotolewa kwa raia.

Kutiwa saini kwa mswada huo kutahakikisha serikali 47 za kaunti zinapokea jumla ya shilingi bilioni 415 katika mwaka huu wa fedha ikilinganishwa na shilingi bilioni 387 zilizopokea mwaka wa fedha uliopita.

“Ongezeko hili kubwa la fedha linaashiria kujitolea kwetu kutafuta rasilimali za kuunga mkono ugatuzi na kuboresha utoaji huduma kwa watu mashinani,” alisema Rais Ruto wakati kutia saini mswada huo katika Ikulu Ndogo ya Homa Bay.

Kongamano la Ugatuzi 2025 ni la tisa kuwahi kuandaliwa tangu kuasisiwa kwa mfumo wa ugatuzi nchini.

Kaulimbiu ya kongamano la mwaka huu ni “Kwa ajili ya Watu, Kwa ajili ya Ustawi: Ugatuzi kama Kichocheo cha Usawa, Ujumuishaji, na Haki ya Jamii.

Kongamano hilo la siku nne litakamilika Ijumaa wiki hii na linawaleta wadau mbalimbali wakiwemo Magavana, Wabunge, Maseneta na Mawaziri ili kuangazia hatua zilizopigwa tangu kuasisiwa kwa mfumo wa ugatuzi nchini.

Share This Article