Kaunti kupata fedha zaidi baada ya Rais Ruto kusaini Mswada wa Ugavi wa Mapato

Martin Mwanje
2 Min Read

Mgao wa fedha kwa kaunti zote 47 kote nchini unatarajiwa kuongezeka kwa takriban shilingi bilioni 30 hadi shilingi bilioni 415 mwaka huu wa fedha. 

Hii ni ikilinganishwa na shilingi bilioni 387 zilizotengewa kaunti katika mwaka wa fedha uliopita.

Hii ni baada ya Rais William Ruto kutia saini Mswada wa Kaunti wa Ugavi wa Mapato, 2025 katika hafla iliyofanyika leo Jumatano asubuhi katika Ikulu ndogo ya Homa Bay.

“Ongezeko hili kubwa la fedha linaashiria kujitolea kwetu kutafuta rasilimali za kuunga mkono ugatuzi na kuboresha utoaji huduma kwa watu mashinani,” alisema Rais Ruto kabla ya kufungua Kongamano la Ugatuzi la mwaka huu litakalofanyika katika kaunti ya Homa Bay.

Wakati wa hafla hiyo iliyoshuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi, Ruto pia alitia saini kuwa sheria Mswada wa Kaunti wa (Marekebisho) ya Sheria za Fedha za Umma, 2023 uliofadhiliwa na Seneta wa kaunti ya Meru Kathuri Murungi.

Mswada huo umefanyia marekebisho Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma ili kutoa fursa ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Mabunge ya Kaunti katika kila kaunti.

Kuongezwa kwa mgao wa fedha kwa kaunti ni habari njema kwa Magavana ambao wamekuwa wakishinikiza kuongezwa kwa fedha zinazotolewa kwa maeneo hayo ya ugatuzi wakisema serikali zao zimeelemewa na mzigo wa majukumu mengi wanayopaswa kutekeleza ili kukidhi mahitaji ya raia.

Share This Article