Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga wamesema waliazimia kushirikiana kuunda serikali jumuishi ili kuhakikisha umoja wa nchi unadumu.
Waliyasema hayo wakati wa mazishi ya mwanaharakati Phoebe Asiyo katika kaunti ya Homa Bay leo Ijumaa.
Rais Ruto akisema kuja kwao pamoja kulikusudia kuhakikisha umoja wa nchi pasi ya kumbagua yeyote kwa misingi ya kikabila, eneo au dini.
“Kwa sababu ya kuja kwetu pamoja, chini ya serikali jumuishi, kwa sababu ya Raila Odinga, akifanya kazi nami na kuunda serikali jumuishi, Kenya ina mustakabali mzuri,” alisema Rais Ruto aliyemlimbikizia Raila sifa sufufu kwa kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya kibinafsi.
“Tumejitolea kuipeleka nchi hadi kiwango kinachofuata.”
Matamshi ambayo pia yalitolewa na Raila aliyesema azimio lake la kufanya kazi na Rais Ruto lilichochewa na kiu ya kuleta uthabiti nchini.
Na kwa wale wenye mashaka, Raila alisema atashirikiana na Rais Ruto hata baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
“Nina imani tutashirikiana hadi baada ya uchaguzi wa 2027. Hakuna anayepaswa kututisha,” alisema kiongozi huyo wa chama cha ODM.
“Kama unasema one term, one term, one term, so what? Ni Wakenya watakaoamua muhula…Wakosoaji wetu tupeni muda na mtuhukumu mwaka 2027.”