Mwanaharakati wa masuala ya kijinsia Phoebe Asiyo atazikwa leo Ijumaa nyumbani kwake wadi ya Kibiri kaunti ya Homa Bay.
Asiyo, ambaye aliaga dunia Julai,16, 2025 Carolina nchini Marekani akiwa na umri wa miaka 90, atakumbukwa kama mama mzalendo, aliyejitolea kuimarisha maisha ya mtoto wa kike hapa nchini.
Asiyo ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Karachuonyo na aliyehudumu wakati mmoja kama rais wa chama cha maendeleo ya wanawake alitajwa sio tu kama mdhamini, bali pia nguzo muhimu kwenye masuala ya wanawake.
Alikuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kwenye baraza la wazee wa jamii ya wa-Luo na alitunukiwa tuzo ya Chief of the Burning Spear mnamo mwaka wa 2018, kwa juhudi zake za kutetea elimu ya mtoto msichana na usawa wa kijinsia nchini Kenya.
Dkt. Asiyo atakumbukwa kwa uongozi bora, upendo na huduma kwa jamii. Alikuwa mkewe marehemu Richard Genga Asiyo.