Watu wanane wafariki kwenye ajali iliyohusisha treni na basi Naivasha

Tom Mathinji
1 Min Read
Watu wanane wafariki kwenye ajali ya Treni Naivasha.

Watu wanane wamefariki na wengine kadhaa wamejeruhiwa baada ya treni kugongana na basi la usambazaji mafuta katika sehemu ya makutano ya Morendat, Naivasha, kaunti ya Nakuru.

Likithibitisha kutokea kwa ajali hiyo Alhamisi jioni, Shirika la Reli Nchini, lilisema ajali hiyo ilitokea wakati basi hilo lilipokuwa likivuka reli.

“Ajali imetokea leo jioni iliyohusisha treni na basi katika kivukio kimoja eneo la Naivasha,” lilisema shirika hilo kwenye mtandao wa X.

Aidha, kulingana na shirika hilo makundi ya uokoaji, wakiwemo maafisa wa polisi na wale wa Shirika la Msalaba Mwekundu walifika katika sehemu ya mkasa upesi kuwasaidia manusura na kudhibiti msongamano wa magari uliosababishwa na ajali hiyo.

“Shirika la Reli Nchini lilipeleka makundi ya uokoaji walioshirikiana na maafisa wa polisi kuwapeleka waliojeruhiwa hospitalini,” iliongeza taarifa ya shirika hilo.

Waliojeruhiwa vibaya walikimbizwa katika hospitali za Naivasha japo wengine walichukuliwa kwa ndege kwa matibabu maalum.

Kampuni ya Kenya Pipeline ambayo maofisa wake walikuwa wameabiri basi hilo ilituma rambirambi zake kwa familia za waathiriwa ni kuhakikishia umma kwamba majeruhi wote wanazingatiwa ipasavyo hospitalini.

Maafisa hao walikuwa wakirejea nyumbai baada ya kukamilisha zamu yao kazini wakati ajali hiyo ilipotokea.

TAGGED:
Share This Article