Wizara ya Fedha imepuuzilia mbali ripoti ya afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliyodokeza kuwa shilingi bilioni 11 zimetoweka kwenye mtandao wa serikali wa eCitizen.
Huku akitaja madai hayo kuwa ya kupotosha, Katibu katika Wizara ya Fedha Dkt. Chris Kiptoo, alikanusha madai kwamba fedha zozote zimepotea tangu jukwaa hilo likabidhiwe kwa serikali mwaka-2023.
Alipofika mbele ya kamati ya Bunge la Taifa kuhusu Uhasibu wa Fedha za Umma siku ya Alhamisi, Katibu huyo alisema jukwaa la E-Citizen linamilikiwa kikamilifu na serikali na habari zake kulindwa na kuhifadhiwa na wizara ya fedha.
Wanachama wa kamati hiyo ambao awali walitaja jukwaa hilo kuwa eneo la uhalifu, walisema watatadhmini majibu ya katibu Kiptoo na kutoa mapendekezo kuhusu jukwaa hilo.
Tangu kuzinduliwa kwake mwaka-2014, jukwaa la e-citizen limekusanya shilingi bilioni- 360 kufikia mwezi Juni mwaka 2025.
Mkakuzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu alikuwa amefichua dosari ya shughuli za kifedha kwenye jukwaa hilo ya shilingi Bilioni 11, hata hivyo akionya kwamba mfumo huo umesababisha ulaghai wa fedha za umma, ufujaji na mianya katika ukusanyaji mapato.