Visa 150 vya ugonjwa wa Kala Azar vyathibitishwa Kajiado

Tom Mathinji
1 Min Read
Kaunti ya Kajiado yavamiwa na ugonjwa wa Kala-azar.

Wakazi wa kaunti ndogo ya Kajiado Magharibi wanakabiliwa na mchipuko wa ugonjwa wa Kala Azar, ambao unasemekana kusambaa katika maeneo mengi ya eneo hilo kame.

Ugonjwa wa Kala Azar unaosababishwa na kimelea cha ‘Leishmania’, huenezwa kwa binadamu kupitia kuumwa na nzi wa kike anayepatikana kwenye maeneo yenye mchanga.

Baadhi ya watu hawana dalili za ugonjwa huo, ilhali kwa baadhi ya wengine, dalili ni pamoja na joto mwilini, kupungua kwa uzani na uvimbe kwenye wengu au ini.

Katika kituo cha matibabu cha Oltepesi, wagonjwa wapatao 150 wametibiwa tangu mwezi Januari, huku wagonjwa 15 wakitibiwa mwezi uliopita.

Vijana wanaochunga mifugo ndio walioathirika zaidi. Wazazi wengi wamelalamikia gharama ya juu ya matibabu katika hospitali za kibinafsi kutokana na dosari za utambuzi.

Idara ya afya katika kaunti ya Kajiado imewaonya wagonjwa kutafuta huduma za matibabu katika kliniki ya afya ya Oltepesi na hospitali ya matibabu maalum ya Kajiado ili kuepusha maafa kutokana na ugonjwa huo.

Share This Article