Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Zambia, Avram Grant, amesema kuwa wamejiandaa ipasavyo kwa fainali za CHAN huku wakifungua dimba leo saa kumi alasiri dhidi ya DR Congo kundini A.
Grant alisema anatumia kikosi chenye chipukizi wengi huku akikitumia kujiandaa kwa siku za usoni.
Kocha huyo alisema kamwe hana shinikizo lolote katika fainali hizi za CHAN.
“Sisi tumefurahia kuwapo hapa Kenya. Tangu tufike tumelindwa vyema, mapokezi mazuri, vyakula vizuri, na tumejiandaa kwa mechi zetu zote za CHAN. Vijana wangu ni wadogo, na ninatumia mashindano hayo kujiandaa kwa mechi zijazo za kimataifa,” alisema Grant.
Zambia almaarufu Chipolopolo watachuana na Chui wa Congo katika mchuano wa kundi A kuanzia saa kumi alasiri katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo.
DR Congo waliopoteza bao moja kwa nunge dhidi ya Kenya watakuwa wakicheza mchuano wa pili huku Zambia, waliowasili nchini Jumatatu wiki hii, wakicheza pambano la kwanza.