Ruto: Hazina ya Hustler haijafeli, imewanufaisha mamilioni ya Wakenya

Hazina ya Hustler ilizinduliwa mwaka 2022 kwa lengo la kutoa mikopo kwa Wakenya wasiojiweza walionyimwa mikopo na taasisi zingine za kifedha nchini.

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto

Rais William Ruto amekanusha madai kuwa Hazina ya Hustler imefeli kabisa kufikia malengo ya uzinduzi wake. 

Hazina hiyo, iliyozinduliwa mwaka 2022, ilikusudiwa kutoa mikopo kwa Wakenya wasiojiweza walionyimwa mikopo hiyo na taasisi zingine za kifedha nchini.

“Wakosoaji wetu…wanasema hivi kwa sababu hawaelewi au wanakataa kukiri ukweli wa kila siku wa mamilioni ya Wakenya ambao hazina hii ilikusudia kuwawezesha,” alisema Rais Ruto aliyezungumza leo wakati wa kikao cha pamoja na wadau wa sekta ya kibinafsi jijini Nairobi.

“Kwao, mkopo wa shilingi 1,000 unaonekana kuwa mdogo mno. Lakini hiyo ni kwa sababu tu kamwe hawajatembea katika viatu vya wale waliotengwa katika jamii kwa muda mrefu.”

Ruto akitumia fursa hiyo kusema kuwa Hazina ya Hustler imewanufaisha Wakenya milioni saba ambao awali walizuiwa na Shirika la Kuhifadhi Takwimu za Watu Wanaoishindwa Kulipa Mikopo (CRB) kupata mikopo.

“Na sasa, wakosoaji wale wale wanaeneza uoga na hali ya kukata tamaa kuwa asilimia 60 ya waliokopeshwa fedha na hazina hiyo wameshindwa kulipa fedha hizo,” alilalama kiongozi wa nchi.

Rais akiweka wazi kuwa hazina hiyo chini ya miaka mitatu imetoa zaidi ya shilingi bilioni 72 kwa Wakenya zaidi ya  milioni 26.

Aliongeza kuwa asilimia 83.3 ya Wakenya waliokopeshwa fedha na hazina hiyo wamelipa mikopo yao, ikikaribia kuwa sawa na sekta ya benki ambayo kiwango cha ulipaji mikopo ni asilimia 83.6.

Kauli zake zinawadia siku chache baada ya ripoti ya Tume ya Kutetea Haki za Binadamu nchini (KHRC) kutilia shaka utendaji kazi wa hazina hiyo kwa misingi kuwa imefeli kabisa kufikia malengo yake.

Ripoti hiyo iliyobaini mfumo wa Hazina ya Hustler ni hafifu ilitoa wito wa kufungwa kabisa kwa hazina hiyo.

Share This Article