Maafisa wa Polisi kutoka kituo cha polisi cha Central Jijini Nairobi, wamewakamata washukiwa wanaohusishwa na mtandao wa wizi wa simu katikati ya Jiji la Nairobi na maeneo yaliyo karibu.
Victor Kimani ambaye ndiye mshukiwa mkuu, alifumaniwa akibadilisha namba maalum za simu (IME), ili kuficha umiliki wake, maafisa hao wa usalama walipofanya operesheni hiyo baada ya kupokea habari za kijasusi.
Baada ya kuhojiwa, Kimani aliwapeleka maafisa hao katika kituo cha kibiashara cha Intermark, ambako washirika wake wawili Marvine Wangundo na Jeremiah Njoroge pia walikamatwa.
Maafisa hao walipofanya upekuzi katika kituo hicho, walipata bidhaa za kielektroniki zinazoshukiwa kuwa za wizi, zikiwa ni pamoja na simu 36 aina ya Samsung, simu 23 aina ya Vivo, mbili za Nokia, moja ya LG, moja ya HMD na sita aina ya M-Kopa Samsung phones, miongoni mwa zingine, huku sehemu za nyuma zikiwa zimetolewa.
Washukiwa hao wanazuiliwa na polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani.