Gavana wa Kisumu Prof. Anyang’ Nyong’o, ametoa wito kwa serikali ya kitaifa kuondolea ushuru vifaa vinavyotumiwa katika utengenezaji wa boti za ‘fiberglass’.
Prof. Nyong’o alisema hatua hiyo itapunguza gharama za uzalishaji na kuharakisha mpito wa Kenya wa matumizi ya vyombo salama vya majini.
Akizungumza wakati wa kuzindua boti tano za uvuvi zilizoundwa kwa vifaa vya fiberglass, mashua ya doria, na maeneo mawili ya kisasa ya kutua kwa boti kwenye eneo la ufuo la Kichinjio katika kaunti ndogo ya Kisumu ya kati, Gavana Nyong’o aliutaja mpango huo kuwa mabadiliko makubwa kwa uchumi wa majini, akiongeza kwamba boti za ‘Fibreglass’ zinatoa usalama ulioimarishwa, udhibiti, na pia kudumu kwa muda mrefu ikilinganishwa na boti za mbao.
“Zikiwa na uwezo wa kubeba kilo 1,500 kwa kila safari, boti hizo zitawawezesha wavuvi watabeba samaki wengi na kuwaongezea mapato. Hatua hiyo itaimarisha maisha yao na kufanikisha utoshelevu wa chakula,” alisema Nyong’o.
Alisema ajali nyingi ziwani zimechangiwa na boti za zamani za mbao, akisema vyombo hivyo vipya vitasaidia kupunguza vifo 5,700 vya kila mwaka ambavyo huripotiwa kwenye Ziwa Victoria.
Gavana huyo aliipongeza kampuni ya ‘Kenya Shipyards Limited’ kwa kutengeneza boti hizo za kisasa humu nchini, akisema ushirikiano huo unahakikisha uwasilishaji kwa wakati na kukuza utaalam wa uhandisi wa baharini.
Mashua hiyo mpya ya doria itasaidia katika utekelezaji wa sheria za uvuvi na ushughulikiaji wa matukio ya dharura.