Serikali ya kaunti ya Kiambu inalenga kuzindua hospitali 32 mpya, kufikia mwezi Disemba mwaka huu ambazo zimegharimu kitita cha shilingi bilioni 2.6.
Gavana wa kaunti ya Kiambu Kimani Wamatangi, amedokeza kuwa ujenzi wa hospitali hizo uko katika hatua za mwisho, zingine zikisubiri kuwekwa vifaa vya afya.
Wamatangi aliyasema hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa hospitali kwenye kaunti hiyo ambazo ni pamoja na Thogoto Level 4, Gathiga, Gitaru, Uthiru, Gichuru, na Hozpitali za Ndeiya Level 3 zilizo katika kaunti ndogo za Kikuyu na Limuru.
Wakati wa ziara hiyo, Gavana huyo alielezea kujitolea kwake kukamilisha ujenzi wa hospitali hizo kuambatana na muda uliowekwa, akipigia debe hatua zilizopigwa tangu achukue hatamu za uongozi wa kaunti hiyo.
“Ndani ya muda wa wiki mbili, tumehakikisha ujenzi wa hospitali hizo unakamilishwa,” alisema Gavana huyo.
Kukamilishwa kwa hospitali hizo kutapunguza msongamano katika hospitali zilizoko na kuleta huduma za afya karibu na wananchi.