Serikali imepuzilia mbali ripoti ya Tume ya kutetea Haki za Binadamu Nchini (KHRC), iliyopendekeza kuondolewa kwa hazina ya Hustler, ikidai hazina hiyo ni ya kisiasa na ya kibaguzi.
Katika mkutano na wanahabari Jumatatu, Waziri wa Vyama Vya Ushirika Wycliffe Oparanya, alitaja matokeo ya ripoti hiyo kuwa ya kisiasa na ambayo hayakuhusisha maoni ya serikali.
Waziri huyo Oparanya alitetea maafikio ya hazina hiyo akisema imebadili maisha ya mamilioni ya wakenya. Alibaini kwamba zaidi ya wakenya milioni 9 wamekuwa wakiomba mikopo kutoka hazina hiyo huku jumla ya wakenya milioni 26 wakiwa tayayari wamekopa kutoka haina hiyo tangu kuzinduliwa.
“Kipindi cha uchunguzi wa ripoti hiyo ni mwaka wa kifedha wa 2022/2023, wakati hazina hiyo ilikuwa imehudumu kwa muda wa miezi saba pekee,” alisema Oparanya.
Kulingana na Oparanya, serikali hutoa shilingi milioni 68 kila siku kama mikopo kupitia hazina hiyo huku juma ya shilingi bilioni 72 zikiwa zimetolewa kufikia sasa.
Ripoti ya tume hiyo iliyotolewa Jana, ilitia doa hazina hiyo ikisema ni ya kisisa tu na wala haijawasaidia wakenya kiuchumi kama ilivyoahidiwa.