Wizara ya Afya imezindua mfumo wa kuthibitisha wagonjwa waliosajiliwa kielekroniki unaolenga kudhibiti ulaghai kwa malipo yanayotolewa chini ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).
Mifumo mingine iliyozinduliwa leo Jumatatu ni app ya wanataaluma wa afya na app ya Practice 360 itakayotumiwa na wahudumu wa afya kuboresha utenda kazi wa SHA.
Mifumo hiyo imezinduliwa wakati kumekuwa na ripoti za malipo ya kutilia shaka ya mamilioni ya pesa yanayodaiwa na hospitali mbalimbali kwa huduma zilizotolewa kwa wagonjwa chini ya SHA.
“Usajili wa kieletroniki kuanzia sasa unatumika katika hospitali za Level 4, 5 na 6 huku juhudi zikiendelea kuzijumuisha hospitali za Level 3 na 2 kote nchini,” alisema Waziri Duale wakati akizndua mfumo huo katika Hospitali ya Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta leo Jumatatu.
“SHA, kuanzia sasa, kamwe haitakubali malipo yaliyoidhinishwa kwa njia ya OTP. Malipo yote ni lazima yaidhinishwe kwa kutumia kitambulisho cha afya cha kielektroniki au app ya Practice 360.”
Waziri Duale alisema tangu ukaguzi wa huduma zilizotolewa na hospitali mbalimbali, SHA imelipa shilingi bilioni 47.5 kwa hospitali mbalimbali na shilingi bilioni 6.9 chini ya mfuko wa afya ya msingi ambao ni wa bure kwa Wakenya wanaopata matibabu katika hospitali za Level 2 hadi 4.
Hadi kufikia sasa, SHA imesajili Wakenya milioni 25.1 huku takriban hospitali, kliniki na vituo vya afya 10,000 vikitoa huduma chini ya mamlaka hiyo.