Usalama umeimarishwa Baringo na Bonde la Kerio, asema Kindiki

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki asema usalama umeimarishwa Baringo.

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amewahimiza viongozi wa eneo la North Rift kuunga mkono juhudi za kudumisha amani huku akitaja hatua zilizopigwa kuwaangamiza majangili na wezi wa mifugo.

Prof. Kindiki alisema tangu utawala wa Kenya Kwanza ulipochukua hatamu za uongozi mwezi Septemba mwaka 2022, walitia bidii kukabiliana na majangili na wahalifu waliowahangaisha wakazi kwa muda mrefu.

Akiwahutubia waumini wa kanisa la AIC Kabartonjo, Baringo Kaskazini alikohudhuria ibada ya Jumapili, Naibu huyo wa Rais alisema Rais William Ruto yuko makini kuhakikisha kuna amani ya kudumu ili kutoa nafasi ya kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo.

“Tumebuni msingi thabiti katika kutafuta amani na usalama maeneo ya Baringo na Bonde la Kerio. Huu ndio msingi ambao Waziri wa sasa wa Usalama wa Taifa anatumia kuhakikisha eneo hili ni salama. Tunamtakia kila la heri,” alisema Kindiki.

Alitoa wito kwa mbunge wa Baringo Kaskazini na mwenzake wa Tiaty William Kamket waliohudhuria ibada hiyo, kuwa mstari wa mbele kuhakikisha upatikanaji wa amani na utangamano wa jamii za maeneo hayo.

Alidokeza kuwa wakazi wa eneo hilo watanufaika na miradi ya maendeleo kutoka kwa serikali, iwapo amani itaendelea kudumishwa.

Share This Article