Wakazi wa Kaunti ya Laikipia, ambayo ina jamii nyingi tofauti, wametakiwa kukataa juhudi zozote za kuwagawanya kwa misingi ya kikabila.
Kiongozi wa chama cha The Service Party (TSP) na Mbunge wa Laikipia Mashariki, Mwangi Kiunjuri, amewataka wakaazi hao kupinga wanasiasa wanaotembelea kaunti hiyo na kuzungumza tu na jamii moja.
Alisisitiza kuwa Laikipia haipaswi kuhusishwa na eneo la Mlima Kenya kwa sababu kijiografia iko katika Mkoa wa zamani wa Bonde la Ufa.
“Laikipia sio Mlima,” Kiunjuri alisema wakati wa hafla ya kuchangisha fedha kwa vikundi zaidi ya 30 vya kijamii katika eneo la Ol Moran, Jimbo la Laikipia Kaskazini. Alikuwa ameandamana na wabunge wengine watano.
Kiunjuri alimkosoa vikali Naibu Kiongozi wa Chama cha DCP na aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, kwa kile alichokiita tabia ya dharau ya mara kwa mara dhidi ya viongozi wanawake.
Akizungumza katika Kambi ya Chifu wa Bombo, mbunge huyo alimlaumu Gachagua kwa kutumia lugha ya kudhalilisha wanawake, akiwa Naibu Rais na sasa akiwa kiongozi wa DCP.
Kwa upande wake mbunge wa Laikipia Kaskazini, Sarah Korere, alikumbuka kufukuzwa katika mkutano na Gachagua kwa kuwa “si mwanachama wa UDA”, huku Mwakilishi wa Wanawake Laikipia, Jane Kagiri, akitusiwa hadharani na Naibu Rais huyo wa zamani kwa “kupeperusha sketi yake Ikulu”, kauli ambayo Kiunjuri aliikemea vikali kuwa ya kudhalilisha sana.
Kiunjuri pia alifichua kuwa amewahi kulengwa binafsi na Gachagua, licha ya kuwa na uhusiano wa kifamilia—kaka yake ameoa katika familia inayohusiana na Gachagua.
Alisema tayari amechukua hatua za kisheria dhidi ya MCA mmoja wa Nyahururu aliyemhusisha na maandamano ya fujo yaliyosababisha uharibifu wa mali katika eneo hilo.
Akimshauri Gachagua kuwa na ukomavu wa kisiasa, Kiunjuri alimtaka amwige Rais wa zamani Mwai Kibaki, ambaye hakuwahi kumshambulia hadharani mtangulizi wake Daniel Moi, licha ya kufutwa kazi kama Makamu wa Rais.
Mbunge wa Tiaty, William Kamket, ambaye pia ana uhusiano wa kindoa na eneo la Mathira, Nyeri, alimshutumu Gachagua kwa mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya wanawake, akisema ni “tabia mbaya isiyofaa kwa kiongozi wa kitaifa.” Kamket aliongeza kuwa hatasita kuunga mkono hoja nyingine ya kumuondoa Gachagua madarakani iwapo nafasi hiyo itajitokeza.
Wakati huo huo, Mwakilishi wa Wanawake wa Laikipia Jane Kagiri, Mwakilishi wa Wanawake wa Samburu Pauline Lenguruis, na Mbunge wa Laikipia Magharibi Wachira Karani walimtetea Rais William Ruto kwa utendakazi wake, wakisema anapaswa kupimwa baada ya kumaliza muhula wake kamili, kama ilivyokuwa kwa marais waliotangulia.
“Ruto anahukumiwa kabla ya miaka mitatu, ilhali marais wengine walitathminiwa baada ya miaka mitano,” walieleza.
Viongozi hao walihitimisha kwa kuwataka wakazi kudumisha amani inayoshuhudiwa kwa sasa katika Kaunti ya Laikipia na kuitumia kama msingi wa kuiunga mkono serikali ya Kenya Kwanza.
MWISHO