CHAN 2024: Katibu Dkt. Omollo, IG Kanja watathmini kiwango cha maandalizi

Martin Mwanje
2 Min Read
Timu ya Baraza la Usalama wa Taifa wakati wa ukaguzi wa viwanja vya Nyayo na Kasarani

Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo akiandamana na Inspekta Mkuu wa Polisi  (IG) Douglas Kanja waliongoza wanachama wa Baraza la Usalama wa Taifa kukagua kiwango cha maandalizi katika viwanja vya Nyayo na Kasarani leo Ijumaa.

Viwanja hivyo vitatumiwa kuandaa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) yatakayong’oa nanga kesho Jumamosi.

Mashindano hayo ya mwezi mmoja yatakamilika Agosti 30.

Wanachama wa baraza hilo walitembelea sehemu za viwanja hivyo ikiwa ni pamoja maeneo ya utenda kazi, vyumba vya kubadilishia nguo na maeneo ya kuingia na kutoka viwanja hivyo.

Timu hiyo ilielezea kuridhishwa kwake na kiwango cha maandalizi kuhusiana na masuala ya usalama, itifaki na matayarisho ya usafiri kwa watakaoshiriki mashindanoni.

Harambee Stars itafungua dimba hilo la CHAN kwa mechi dhidi ya DR Congo Jumapili hii, kuanzia saa tisa alasiri katika mchuano wa kundi A.

Mechi nyingine za kundi A, kando na mechi nne za Harambee Stars, zitasakatwa katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo.

Kenya itaandaa mechi 12 za kipute hicho ikiwemo fainali ya Agosti 30.

Wenyeji wenza Tanzania wataandaa mchuano wa ufunguzi kundini B Jumamosi hii dhidi ya Burkina Faso katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mashindano ya CHAN yanaandaliwa kwa pamoja na Kenya, Tanzania na Uganda.

Usikose kutazama runinga ya KBC Channel 1 kwa uhondo wa mashindano hayo ambayo pia matangazo yake yatapeperushwa kwenye idhaa za redio za KBC.

Share This Article