Mataifa ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda yamefanya mazungumzo yao ya kwanza baada ya kutia saini makubaliano ya amani ya kumaliza mgogoro uliodumu miongo kadhaa.
Mgogoro huo umeikumba mashariki ya DRC ambayo ina utajiri mkubwa wa madini.
Mataifa hayo mawili yalisema leo Ijumaa kuwa mazungumzo kati yao yameng’oa nanga.
“Julai 31, 2025, wawakilishi kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Jamhuri ya Rwanda (Rwanda), pamoja na waangalizi” walifanya mkutano wao wa kwanza mjini Washington tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya amani katika mji huo mkuu wa Marekani Juni 27,” ilisema taarifa ya pamoja iliyotolewa na mataifa yote mawili kwenye mitandao ya kijamii leo Ijumaa.