Wizara ya Afya: Visa 314 vya Mpox vimethibitishwa nchini

Kaunti ya Mombasa inaongoza kwa idadi ya visa 146, Busia (63), Nakuru (21), Kilifi (19), Nairobi (17) na kaunti ya Makueni visa 13.

Martin Mwanje
2 Min Read

Juma ya visa 314 vya ugonjwa wa Mpox vimethibitishwa kote nchini hadi kufikia sasa. 

Hii ni tangu kuanza kwa mlipuko wa ugonjwa huo mwezi Julai mwaka 2025.

Kulingana na takwimu za Wizara ya Afya, kaunti ya Mombasa inaongoza kwa idadi ya visa 146 kati ya kaunti 22 zilizothibitishwa kuathiriw na ugonjwa huo.

Kaunti ya Busia inafuata kwa visa 63, Nakuru (21), Kilifi (19), Nairobi (17), Makueni (13), Taita Taveta na Uasin Gishu visa 5 kila moja huku kaunti ya Bungoma ikithibitishwa kuwa na visa 4 vya ugonjwa huo.

Kaunti za Kajiado, Kiambu na Kakamega zimeripoti visa 3 kila moja huku kaunti za Kericho na Machakos zikiripoti kisa kimoja kila moja.

Kwa upande mwingine, kisa kimoja cha Mpox kimeripotiwa katika kila kaunti za Migori, Kisii, Kirinyaga, Isiolo, Kitui, Narok, Baringo na Trans Nzoia.

“Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, visa vinne zaidi vya ugonjwa wa Mpox vimeripotiwa katika kaunti za Mombasa (3) na Nairobi (1),” amesema Waziri wa Afya Aden Duale kwenye taarifa.

Jumla ya watu 33 wamelazwa na wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali mbalimbali kutokana na ugonjwa huo huku wengine 54 wakitengwa na kutibiwa nyumbani.

Wagonjwa 222 wamepona kabisa.

Waziri Duale akisema wizara yake kwa ushirikiano na serikali za kaunti zimeimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huo kote nchini na kuutaka umma kuchukua hatua za kuzuia msambao wake.

Hatua hizo zinajumuisha kutotangana na watu walioambukizwa ugonjwa huo, kutotumia vitu sawa na watu walioambukizwa, kunawa mikono mara kwa mara na kupiga ripoti haraka kwenye kituo cha afya kilicho karibu nawe ili upate matibabu punde unapobaini kuwa na dalili za ugonjwa huo.

Share This Article