Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru ametoa wito kwa Serikali ya Taifa kununu mchele unaokuzwa hapa nchini, kabla ya kuagiza mchele kutoka nje ya nchi bila ushuru.
Waiguru alisema kuwa huku ikifahamika kuwa taifa hili halikuzi mchele wa kutosha kukidhi mahitaji ya nchi, ni vyema wakulima wa hapa nchini wapewe kipaumbele.
Alionya kuwa mpango wa kuagiza metrik tani 500,000 za mchele kutoka nje, jinsi ilivyotangazwa na Waziri wa Fedha John Mbadi, huenda utawaathiri wakulima wa mchele wa Mwea.
“Kabla ya kuagiza mchele kutoka nje, ni vyema kufahamu kuwa maghala yetu yamejaa pomoni, na tunawahimiza kwanza mnunue mchele huo kisha muagize kutoka nje ili kujaza nakisi,” nalisema Waiguru.
Wito wa Gavana huyo unajiri baada ya Waziri wa Fedha kuchapisha kwenye Gazeti Rasmi la Serikali agizo la kuingiza mchele hapa nchini bila kutozwa ushuru kabla ya Disemba 31,2025.
Hatua hiyo imelaumiwa na wakulima wa mchele eneo la Mwea, amboa wana wasiwasi kwamba mchele huo ambao hautozwi ushuru utafurika kwenye masoko ya hapa nchini na kudumaza uzalishaji wa hapa nchini.
Aidha Waiguru alidokeza kuwa uagizaji wa mchele hapa nchini bila kutozwa ushuru, unapaswa kutekelezwa baada ya kununuliwa kwa mchele unaokuzwa hapa nchini.