Katibu wa Idara ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabia nchi Dkt. Mhandisi Festus Ng’eno, amemteua Edward Maina Muriuki kuwa kaimu Mkurugendi wa Huduma za utabiri wa hali hewa.
Muriuki anachukua wadhifa huo kufuatia kustaafu kwa Dkt. David Gikungu.
Muriuki ana shahada ya uzamili ya sayansi kwenye masuala ya uhandisi wa maji kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, stashada ya uzamili kwenye masuala ya Hydrology na shahada ya hisabati na utabiri wa hali ya hewa kutoka chuo kikuu cha Nairobi.
Alijiunga na Huduma ya Utabiri wa Hali ya Hewa mwaka 1991, na kufanya kazi kwa kitengo cha kiufundi na usimamizi, kaatibu wa Shirika la kanda la mafunzo ya Huduma za Utabiri wa Hali ya Hewa na Naibu Mkurugenzi wa Huduma za utabiri.
“Uteuzi huu unaashiria hatua kubwa katika taaluma yangu mpya,” alisema Maina.
Aliahidi kushirikiana na wafanyakazi wote katika idara hiyo na washirika wake ili kuboresha utoaji huduma za masuala ya anga.
Kaimu mkurugenzi huyo alisema hitaji linaloongezeka la habari kuhusu hali ya anga na wito wa jamii ya kimataifa wa kutekelezwa kwa mfumo wa utoaji onyo za mapema zitakuwa nguzo kuu za usimamizi wake katika idara hiyo.