Kenya yalalamika rasmi kwa EAC kuhusu sheria mpya ya kibiashara ya Tanzania

Tom Mathinji
2 Min Read
Katibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Caroline Karugu.

Kenya imeiandikia rasmi sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kuhusu hatua ya hivi majuzi ya serikali ya Tanzania ya kuwazuia raia wa kigeni dhidi ya kufanya baadhi ya biashara, ikisema hatua hiyo inahujumu utangamano wa kiuchumi wa kanda hii.

Kupitia kwa taarifa iliyotolewa Jumatano, katibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Caroline Karugu, alisema maagizo hayo yanakinzana na Itifaki ya Soko la Pamoja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, inayowapa haki raia wa Jumuiya hiyo kuanzisha biashara na utoaji wa huduma katika kanda hiyo.

“Agizo hilo linadumaza lengo kuu la utangamano wa kiuchumi na kuhujumu mafanikio chini ya Itifaki za Soko la Pamoja la EAC,” alisema Dkt. Karugu.

Alisema Kenya imechukua hatua rasmi katika kiwango cha kanda kwa kuiandikia sekretriati  ya EAC kuingilia kati kuhusu swala hilo.

“Lengo la barua hii ni kutaka EAC ichukue hatua ya kuifahamisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba agizo lake linakiuka makubaliano ya EAC, sheria za Jumuiya hiyo na pia linakiuka Itifaki za Soko la Pamoja la EAC,” ilisema sehemu ya barua hiyo kwa Katibu Mkuu wa EAC Veronica Nduva.

Agizo hilo jipya la Tanzania linawazuia raio wasio wa taifa hilo dhidi ya kujihusisha na aina 15 za biashara, zikiwemo za rejareja, viwanda vya huduma na biashara ndogo ndogo.

Aidha sheria hiyo mpya imeagiza kuto-toa upya leseni za biashara za wafanyabiashara wasio raia wa Tanzania katika sekta zilizoathiriwa.

Watakaokiuka agizo hilo watatozwa faini isiyozidi shilingi milioni 10 za Tanzania, kifungo cha hadi miezi sita gerezani na kufutiliwa mbali kwa visa na idhini za makazi.

Share This Article