Agai na JOBO kumenyana kwenye nusu fainali

Martin Mwanje
1 Min Read

Kivumbi kikali kinatarajiwa kutifuka hapo kesho wakati shule ya wavulana ya Agai itakapokabana koo na ile ya St. Joseph (JOBO) katika nusu fainali ya mashindano ya kitaifa baina ya shule za upili yanayoendelea katika kaunti ya Kakamega.

Timu hizo zilifuzu hatua hiyo baada ya kumaliza kwenye nafasi ya pili na ya kwanza mtawalia kwenye makundi yao.

Mchuano huo wenye halaiki ya mashabiki huenda ukasakatwa katika uga wa Mumias ulio na uwezo wa kukimu halaiki hiyo.

Vile vile, kutagaragazwa nusu fainali nyingine baina ya wenyeji Musingu walioongoza kundi A na mabingwa watetezi Highway waliomaliza wa pili kwenye kundi B.

Kwenye mechi zao za mwisho za makundi, Musingu waliwaadhibu Agai goli moja kwa nunge nao Highway wakawalaza Serani mabao mawili kwa sufuri.

Kwenye kitengo cha vipusa, mabingwa watetezi Butere watakabiliana na Kobala nao Madira wamalize udhia dhidi ya Nasokol.

Mitanange hiyo minne itachezwa kabla ya saa saba mchana ili kutoa nafasi kwa timu hizo kupumzika na kujiandaa kwa fainali siku ya Jumamosi.

TAGGED:
Share This Article