CHAN 2024: Timu za mashinani kutoka Laikipia na Nyandarua zina hamu ya kujifunza

Martin Mwanje
3 Min Read

Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) yanatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii, na timu za soka kutoka kaunti za Laikipia na Nyandarua zina hamu kubwa ya kunufaika na kujifunza kutoka kwa mataifa mbalimbali ya Afrika yatakayoshiriki.

CHAN ni mashindano ya soka yanayoandaliwa kila baada ya miaka miwili na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), ambapo hujumuisha tu wachezaji wanaocheza katika ligi za ndani ya nchi zao.

Katika mji wa Nyahururu, wachezaji wa Barcelona FC wakiongozwa na Nahodha Lenjiloti Kyle na Msaidizi wake Martha Simiyu walisema wana hamu kubwa ya kuona na kujifunza kutoka kwa timu zitakazoshiriki.

“Tunasubiri kwa hamu mashindano ya CHAN. Ni fursa nzuri ya kujifunza na kujikuza kisoka,” alisema Kyle.

Naye Martha Simiyu aliongeza, “Tunawahamasisha wasichana wachanga kuunda vilabu vya soka. Mpira wa miguu ni mchezo unaowaunganisha watu. Tunajifunza mengi kutoka kwa wachezaji wenzetu kila siku.”

Katika eneo la Kinangop, kaunti ya Nyandarua, Kocha Dan Musomba ambaye huifundisha timu ya Shule ya Sekondari ya Muruaki pamoja na All Stars FC ya Nyahururu, alisifu serikali kuu kwa ukarabati na uboreshaji wa viwanja vya Nyayo na Kasarani ambavyo vitatumika kwa mechi za CHAN mwezi wa Agosti.

“Ninaipongeza serikali kwa kazi nzuri ya kukarabati viwanja hivyo muhimu. Ni heshima kubwa kwa Kenya kuwa mwenyeji wa mashindano haya ya bara,” alisema Musomba.

Pia alitoa wito kwa Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) kuhakikisha linaonyesha mechi zote za CHAN moja kwa moja kupitia KBC Channel One, hasa kwa wananchi ambao hawatakuwa na uwezo wa kununua tiketi za kuingia uwanjani.

“Watu wengi hawatapata nafasi ya kuhudhuria viwanjani, hivyo ni muhimu KBC watangaze ratiba mapema na kuhakikisha mechi zinaonyeshwa moja kwa moja kwa wananchi wote,” alisema.

Kocha Musomba aliwahimiza vijana kuonyesha upendo na amani kwa wageni wakati wa mashindano hayo.

“Huu si wakati wa porojo za kisiasa. Ni wakati wa kujifunza kutoka kwa timu za mataifa mengine. Sisi kama makocha na timu za mashinani tunapaswa kutumia fursa hii kujikuza.”

Mashindano ya CHAN 2025 yanapowadia, timu kama vile Barcelona FC ya Nyahururu na shule ya sekondari ya Muruaki ya Kinangop zina matumaini makubwa ya kubadilika kisoka kupitia uzoefu na mafunzo kutoka kwa mashindano haya ya bara.

Share This Article