Wawakilishi Wadi Isiolo wakanusha madai ya kupitisha bajeti ya shilingi bilioni 7 kwa udanganyifu

Martin Mwanje
5 Min Read

Baadhi ya Wawakilishi Wadi (MCAs) wa kaunti ya Isiolo wamekana vikali madai kwamba walipitisha bajeti ya shilingi bilioni 7 ya mwaka wa fedha wa 2025/2026 kwa njia ya udanganyifu, wakiyataja madai hayo kuwa ya kupotosha, si ya kweli, na yenye misukumo ya kisiasa.

Wakiongozwa na Naibu Spika ambaye pia ni MCA wa Wadi ya Oldonyiro, David Lemantile, wawakilishi hao walisema kuwa mchakato wa bajeti ulifuata sheria na taratibu zote za kisheria, na wakawatahadharisha wakazi wa Isiolo dhidi ya kupotoshwa na watu wanaotaka kuvuruga amani na maendeleo ya kaunti hiyo.

Awali wiki hii, kundi la MCAs wanaomuunga mkono aliyekuwa Spika Mohamed Roba Qoto ambaye aliondolewa kwa njia tata na nafasi yake kuchukuliwa na Abdullahi Banticha Jaldesa kufuatia jaribio lililofeli la kumng’oa madarakani Gavana Abdi Guyo, walidai kuwa bajeti hiyo ilipitishwa kwa njia ya ulaghai na wafuasi wa serikali ya Gavana Guyo bila kufuata utaratibu unaostahili.

Hata hivyo, katika majibu ya haraka, MCAs wanaomuunga mkono Gavana Guyo wakiongozwa na Lemantile walikanusha madai hayo wakisema hayana ukweli wowote na ni propaganda za kisiasa zinazolenga kukwamisha utoaji wa huduma kwa wakazi wa Isiolo kwa kisingizio kuwa serikali haifanyi kazi.

Lemantile aliwahimiza wakazi kudumisha umoja na amani, na kuwa makini ili wasitumiwe na wanasiasa wachache kwa maslahi yao binafsi kuvuruga utulivu wa kaunti hiyo.

“Hatutakuwa na kaunti nyingine ya kukimbilia. Tuwe watu wa amani. Kila mtu afanye kazi yake. Kama kuna jambo haliko sawa, zipo njia za kisheria za kulitatua,” alisema Lemantile.

Alisisitiza kuwa Bunge la Kaunti lilipokea Mswada wa Ugavi wa Fedha wa 2025/26 kwa mujibu wa Kanuni ya 222(1) ya Bunge, na uliidhinishwa baada ya kupitia athari zake kwa maendeleo, uwekezaji, ajira, na ukuaji wa uchumi.

“Serikali ya kaunti ya Isiolo iko ndani ya sheria kuanza utekelezaji wa Sheria ya Ugavi wa Fedha ya mwaka 2025 kama ilivyochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali,” alieleza Lemantile.

Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Ugavi wa Fedha, Rehema Abdikadir, naye alikubaliana na kauli ya Lemantile akisema madai kuwa bajeti ilipitishwa bila kufuata sheria si ya kweli na yanalenga kuleta hofu na migawanyiko isiyo na sababu.

“Nawahakikishia wakazi wa Isiolo kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 ilipitishwa kwa kufuata hatua zote za kisheria. Hatukupuuza chochote. Kila hatua ilifuatwa ipasavyo,” alisema Rehema.

Aliwataka wakazi wawe waangalifu na wasikubali kupotoshwa na propaganda zinazoenezwa na watu wanaotaka kuvuruga utenda kazi wa serikali ya kaunti na kuhujumu utoaji wa huduma.

“Kama naibu mwenyekiti wa kamati, ninathibitisha kuwa mchakato wote ulikuwa wa haki na wa kisheria. Serikali lazima iendelee kufanya kazi na kutoa huduma kwa wananchi,” aliongeza.

MCA aliyechaguliwa kwa uteuzi maalum, Francis Letimalo, alitetea mchakato huo wa kupitisha bajeti akisema kuwa bajeti hiyo iliidhinishwa na MCAs tisa kati ya 18, idadi ambayo iko juu ya kiwango cha chini cha MCAs sita kinachohitajika kwa kikao cha bunge kuwa halali.

“Wanaosema kuwa bajeti haikupitishwa kihalali si wakweli. Tulikuwa na idadi ya kutosha. Wengine walikuwa kwenye migogoro ya kisiasa, sisi tukafanya kazi yetu,” alisema Letimalo.

Aliongeza kuwa kamati ya bajeti pamoja na vikao vya bunge vilikuwa halali na viliendeshwa kwa kufuata sheria.

“Mchakato ulikuwa wa haki, halali, na uliofuata taratibu,” alisisitiza Letimalo.

Kwa upande mwingine, kiongozi wa wengi katika Bunge la Kaunti na MCA wa Wadi ya Garbatula, Abdirashid Ali, alielezea wasiwasi wake kuhusu hali ya utovu wa usalama inayoendelea kushuhudiwa katika majengo ya bunge hilo, ambapo watu wasiojulikana wamekuwa wakilinda majengo hayo kwa silaha mbalimbali badala ya maafisa wa polisi.

Aliitaka timu ya usalama ya kaunti kuingilia kati na kuwaondoa watu hao wenye silaha kutoka eneo la bunge la kaunti, akisisitiza kuwa kuna njia za kisheria ambazo mtu yeyote aliye na malalamiko anapaswa kuzitumia kutafuta haki.

TAGGED:
Share This Article