Waziri wa Afya Aden Duale, ametangaza mikakati ya dharura inayotekelezwa ili kuimarisha usalama, uwajibikaji na utunzaji bora wa wagonjwa katika hospitali zote za rufaa hapa nchini.
Hatua hiyo inajiri baada ya wagonjwa wawili kufariki kwenye Hopsitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) kwa njia tatanishi, na kuibua wasiwasi kuhusu usalama wa wagonjwa wakiwa hospitalini.
“Kama wizara tuna jukumu la kulinda maisha, haki na heshima ya wagonjwa wote. Tumejitolea kuhakikisha visa kama hivyo havitokei tena,” alisema waziri Duale.
Duale aliyasema hayo leo Jumatatu, baada ya kufanya ziara katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), kutathmini mianya iliopo na kupanga mabadiliko ya dharura ili kurejesha imani ya umma katika mfumo wa afya.
Miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni pamoja na kuwaruhusu wageni wawili tu kwa kila mgonjwa, wageni wote watafanyiwa upekuzi wanapoingia kwenye hospitali hiyo, kuimarisha mifumo ya kushughulikia malalamishi, utoaji wa mafunzo kwa wahudumu wa afya kuhusu haki za wagonjwa na viwango vya usalama, na kuongeza doria za kiusalama kwa wagonjwa.
Wakati huo huo, waziri huyo aliagiza hospitali kushirikiana kwa karibu na wizara ya Usalama wa Taifa, Machifu na viongozi wa kijamii ili kuwasaidia wagonjwa waliotelekezwa hospitalini.
Kulingana na Duale, hatua hiyo inajumuisha kuwatafuta jamaa wao, kuwaruhusu kuondoka hospitalini kwa njia ya heshima na kuwapeleka waliotelekezwa kwenye taasisi za kuwatunza watu iwapo juhudi za kuwatafuta jamaa wao zitagonga mwamba.
“Juhudi hizo zinalenga kurejesha heshima na kuimarisha uwajibikaji. Kila mgonjwa ana haki ya kushughulikiwa kwa utaalam na heshima,” aliongeza Duale.
Duale alirejelea kujitolea kwa wizara yake kuendelea kuimarisha utoaji huduma, akidokeza kuwa usalama na imani ya umma zimepewa kipaumbele.