Kongamano la Taifa la Ugonjwa wa Saratani liling’oa nanga leo Jumatatu huku wadau wakitoa wito wa juhudi zaidi kufanywa ili kutambua ugonjwa wa saratani mapema kwa lengo la kuudhibiti.
Kaulimbiu ya kongamano hilo la siku tatu na ambalo ni la pili kuwahi kufanyika nchini ni “kuunganisha sauti zetu na kuchukua hatua.”
Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi alizindua rasmi kongamano la mwaka huu linalofanyika jijini Nairobi, likiwaleta pamoja wataalam wa afya ili kutafuta mbinu za kuupiga dafrau ugonjwa wa saratani ambao unaendelea kusababisha vifo ya maelfu ya watu kila mwaka.
“Saratani inaendelea kuwa changamoto siyo tu humu nchini bali pia kote duniani,” alisema Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.
Mudavadi akisema kuna haja ya ushirikiano wa wadau wote ili kuhakikisha juhudi za kuushinda ugonjwa huo zinazaa matunda.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Afya Aden Duale aliuita ugonjwa wa saratani kuwa siyo tu janga la afya bali pia dharura ya kitaifa.
Duale akidokeza kuwa kila mwaka, Wakenya 120,000 hubainika kuwa na ugonjwa huo huku wagonjwa 29,000 wakifariki.
Waziri alisema serikali ya Kenya Kwanza iko mbioni kuhakikisha vifaa vinavyohitajika vinawekwa katika hospitali za umma kote nchini ili kusaidia kutambua ugonjwa huo mapema na hivyo kuokoa maisha ya waathiriwa.
“Hakuna Mkenya anayepaswa kuteseka au kufariki kwa sababu ya kuchelewa kupata matibabu,” aliongeza Duale.
Kulingana na Waziri huyo, zaidi ya asilimia 7o vya visa vya ugonjwa wa saratani huripotiwa kuchelewa, hali inayofanya iwe vigumu kuutibu ugonjwa huo.
Alitoa wito kwa Wakenya kujiandikisha na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) ili kuhakikisha wanapata huduma bora za afya zitakazosaidia katika kuukabili ugonjwa wa saratani nchini.
Gavana wa Kisumu Prof. Anyang’ Nyong’o kwa upande wake alipongeza mikakati mbalimbali iliyowekwa na serikali ili kukabiliana na saratani.
Hata hivyo, alionya kuwa mikakati tu bila kuchukua hatua stahiki haitazaa matunda.
“Ni wakati wa vitendo, siyo kuratibu sera tu,” alishauri Prof. Nyong’o ambaye mwenyewe ni mwathiriwa wa saratani.
Alisisitiza umuhimu wa kufanya vipimo vya kutambua ugonjwa wa saratani mapema, ikiwa ni pamoja na saratani ya matiti na ya mlango wa uzazi.
Wito sawia ulitolewa na Dkt. Githinji Gitahi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Amref Health Africa.
Dkt. Gitahi alisisitiwa kuwa vita dhidi ya ugonjwa wa saratani vitafanikiwa tu ikiwa utatambuliwa na kutibiwa mapema na ikiwa vifaa tiba vya ugonjwa huo vitapatikana kwa urahisi hospitalini.
Alilalamikia idadi ndogo ya wasichana wenye umri kati ya miaka 10 hadi 14 waliopewa chanjo ya HPV nchini, wakati idadi hiyo inapaswa kuwa takriban asilimia 80.
Chanjo hiyo husaidia kuzuia saratani ya mlango wa uzazi.