Marekani na Umoja wa Ulaya, EU zimefikia makubaliano ya biashara na kumaliza mivutano iliyodumu miezi kadhaa kati ya pande hizo mbili.
Rais Donald Trump, aliyezungumza baada ya mkutano kati yake na Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen huko Scotland jana Jumapili, amesema amefikia makubaliano ya ushuru wa forodha wa asilimia 15 kwa bidhaa zote za EU zitakazoingizwa nhini Marekani.
Hii ilibainika baada ya wawili hao kuwahutubia wanahabari punde baada ya mkutano wao.
Trump alikuwa ametishia kuzitoza bidhaa za EU ushuru wa forodha wa asilimia 30 kuanzia Ijumaa, makataa aliyoweka ya makubaliano kufikiwa kabla ya ushuru huo kuanza kutekelezwa.
Hata hivyo , Rais huyo wa Marekani amesema hakutakuwa na mabadiliko kwenye ushuru wa asilimia 50 unaotozwa chuma na alumini zinazoingia nchini Marekani.
Ameongeza kuwa Umoja wa Ulaya utanunua nishati yenye thamani ya dola bilioni 750 kutoka nchini Marekani na kisha kufanya uwekezaji mpya wa dola bilioni 600 nchini humo.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi zote za EU zitafungua masoko yake kwa Marekani bila ushuru.
Kwa upande wake, Von der Leyen amesema wamefikia makubaliano hayo ya biashsara yataleta uthabiti na hali ya kutabirika.