Wakulima wa miwa hapa nchini wana sababu ya kutabasamu, kufuatia hatua ya serikali kuongeza bei ya tani moja ya miwa kutoka shilingi 5,500 hadi shilingi 5,750.
Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo Mutahi Kagwe, alitangaza bei hiyo mpya akidokeza kuwa hatua hiyo iliidhinishwa na kamati ya muda, wakati wa kikao chake cha pili Julai 17,2025.
Kulingana na Kagwe, bei hiyo mpya itaanza kutekelezwa Julai 21,2025.
“Baada ya kukadiria bei ya miwa kwa muda wa miezi mitatu iliyopita (Aprili – Juni 2025), kamati hiyo iliidhinisha nyongeza ya bei ya miwa kutoka bei ya sasa ya shilingi 5,500.00 kwa kila tani hadi shilingi 5,750.00 kwa kila tani, kuanzia Julai 21,2025.” alisema waziri Kagwe.
Waziri Kagwe alisema hatua hiyo inaambatana na juhudi za serikali za kuimarisha sekta ya kilimo, na kufanikisha kufidiwa kwa wakulima ambao ndio uti wa mgongo wa sekta ya sukari hapa nchini.
“Nyongeza hiyo itaboresha udhabiti wa kifedha na kuwapa motisha wakulima wakati wa msimu wa upanzi. Wakulima wa miwa sasa wataenda kwa benki wakiwa na tabasamu,” alidokeza waziri huyo.