Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania utaandaliwa Oktoba 29, 2025, hayo ni kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) nchini humo Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacob Mwambegele.
Jaji Mwambegele alisema maandalizi ya uchaguzi huo yameanza rasmi na kuainisha tarehe muhimu katika kalenda ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, utoaji wa fomu za uteuzi kwa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais utafanyika kati ya Agosti 9 na 27, 2025.
Aidha, ameongeza; “Tarehe 27 Agosti 2025 itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa kiti cha rais na makamu rais, uteuzi wa wagombea ubunge na uteuzi wa wagombea udiwani”, alisema Jaji huyo.
Kwa upande wa kampeni, Tanzania Bara itakuwa na kipindi cha kampeni kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 28, huku Tanzania Zanzibar kampeni zikiendeshwa kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 27, ili kupisha upigaji wa kura ya mapema.