Katibu Mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna sasa anasema yuko tayari kuachia ngazi kama Katibu Mkuu wa chama cha ODM ikiwa atatakiwa kufanya hivyo.
Sifuna, ambaye pia ni Seneta wa kaunti ya Nairobi, amekuwa mkosoaji mkali wa serikali ya Kenya Kwanza ambayo imeingia kwenye muungano na chama chake cha ODM.
Hatua hiyo imewafanya baadhi ya vigogo wa ODM kutaka Sifuna afurushwe kwenye wadhifa huo wakidai anakiuka maadili ya chama.
“Mimi ni mfanyakazi wenu. Siwezi kuwa Katibu Mkuu ambaye wanachama wa ODM hawataki akuwe pale. Kuna watu kwa hii chama hawajui Sifuna alitoka wapi, na alikujaje akakuwa Katibu. Mimi sitawasikiza wale. Kuna watu wanajua vile Sifuna alijipata kwa hii kiti. Hao watu, akiwemo huyu Baba Raila Amolo Odinga, siku ile wataniambia Sifuna sasa wewe umeanza kuwa na maadili tofauti na chama, nitawaachilia hii kiti bila fujo,” alisema Sifuna wakati akiwahutubia wajumbe wa ODM katika kaunti ya Kakamega leo Ijumaa.
Wajumbe hao wakimtaka Sifuna kamwe kutojiuzulu wadhifa huo na badala yake kuendelea kusema ukweli jinsi afanyavyo kuhusiana na utenda kazi wa serikali ya Kenya Kwanza.