Ufadhili wa elimu ya msingi bila malipo: Wadau watoa maoni mseto

Waziri wa Fedha John Mbadi amesema serikali kamwe haiwezi kuendelea kufadhili kikamilifu elimu ya msingi bila malipo nchini. Wadau wanahofia hatua hiyo itakuwa na madhara makubwa kwa sekta ya elimu.

Martin Mwanje
2 Min Read
John Mbadi - Waziri wa Fedha

Viongozi mbalimbali wameendelea kutoa maoni mseto kuhusiana na hatua ya serikali kutangaza kuwa kamwe haitafadhili kikamilifu elimu ya msingi bila malipo katika shule za umma nchini. 

Hayo yalisema na Waziri wa Fedha John Mbadi jana Alhamisi alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Taifa juu ya Elimu kujibu masuali kuhusiana na sekta ya elimu nchini.

Mbadi akiungama kuwa serikali haina fedha za kutosha kuendelea kufadhili kikamilifu mpango wa elimu ya msingi bila malipo.

Mpango huo ulianzishwa na utawala wa aliyekuwa Rais wa nchi hii, Hayati Mwai Kibaki.

Chama cha KUDHEIHA kimeelezea hofu kuwa hatua hiyo itawanyima wanafunzi wengi, hasa kutoka familia maskini, haki ya kupata elimu bora na ya gharama nafuu.

Katibu Mkuu wa chama hicho Albert Njeru ametoa wito kwa serikali kubatilisha hatua hiyo anayosema itakuwa na madhara makubwa kwa sekta ya elimu nchini.

Kauli sawia zimetolewa na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

“Mambo ya Free Basic Education, hatumwomba mtu yeyote. Tunasema ni lazima mpango huo uendelee,” alisema Nyoro ambaye wakati mmoja alikuwa mwenyekti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Taifa.

“Hatutakubali yeyote kufanya mchezo na suala la elimu ya msingi bila malipo. Chumi hujengwa na watu, kazi ya elimu ni kuongeza thamani kwa watu, kwa wafanyakazi katika mantiki ya kiuchumi. Elimu huongeza thamani kwa wafanyakazi ambao ni watu, na uchumi wa Kenya unaweza kukua tu ikiwa elimu itapatikana kwa wote, ni elimu bora na kila mtu ako na fursa ya kuipata,” aliongeza mbunge huyo aliyezungumza katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, CUEA.

Waziri wa zamani wa Elimu Dkt. Fred Matiang’i, akigusia suala hilo alipendekeza kusitishwa kwa baadhi ya mipango inayotekelezwa na serikali kama ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ili fedha zinazotumiwa kwenye mipango hiyo zitumiwe kufadhili mpango wa elimu bila malipo nchini.

Matiang’i ambaye ametangaza azima yake ya kuwania urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2027 ameahidi kurejesha ufadhili kamili wa mpango wa elimu bila malipo ikiwa atapewa fursa ya kuiongoza nchi.

 

 

 

 

 

Share This Article