Wetang’ula: Wakenya wanaoishi ng’ambo waendelee kutuma fedha nchini

Martin Mwanje
1 Min Read
Moses Wetang'ula - Spika wa Bunge la Taifa

Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula anasema Kenya inapaswa kufanywa kuwa thabiti kiuchumi ikiwa ni pamoja na kwa kutumia fedha zinazotumwa kutoka ughaibuni.

Wetang’ula amewataka Wakenya hasa wanaoishi nchini Marekani kukataa ushauri wa kupotosha unaotolewa na viongozi wasiokuwa na maono.

Kulingana naye, viongozi wanaowashauri Wakenya wanaoishi ughaibuni kutojenga nchi yao wamepoteza mwelekeo.

“Kenya ni nyumbani na fedha zinazopokelewa kutoka ng’ambo katika dola hutumiwa kuufanya uchumi kuwa thabiti kupitia ubadilishanaji wa fedha za kigeni,” alisema Wetang’ula  wakati wa mkutano wa uwezeshaji ulioandaliwa katika uwanja wa Nyamache, kaunti ya Kisii leo Ijumaa.

Aliwapongeza wakazi wa Kisii wanaoishi ng’ambo kwa kuwa mstari wa mbele katika kutuma fedha nchini, fedha alizosema zimebadilisha taswira ya eneo hilo kupitia maendeleo.

Matamshi yake yanakuja wakati ambapo Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua yupo kwenye ziara nchini Marekani.

Kwenye ziara hiyo, Gachagua ameikosoa vikali serikali ya Kenya Kwanza akidai imeshindwa kuchapa kazi na kufanya Wakenya kuelemewa na gharama ya juu ya maisha.

Share This Article