NCIC: Mazungumzo baina ya vizazi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi

Tom Mathinji
2 Min Read

Mazungumzo baina ya vizazi yatapiga jeki maendeleo ya taifa hili na kufanikisha udumishaji amani na maridhiano, hayo yamesemwa na Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uwiano na Utangamano Dkt. Danvas Makori.

Akizungumza leo Alhamisi katika kaunti ya Marsabit, Dkt. Makori alisema kuna maswala kadha ambayo kwa muda mrefu yamesalia bila kusuluhishwa na kusababisha taharuki hapa nchini.

“Maandamano ya mwaka 2024, yaliyosababishwa na Mswada wa Fedha yalizuka, lakini kulikuwa na maswala mengi ambayo kwa muda mrefu hayakuwa yameshughulikiwa. Tuligundua kulikuwa na tatizo, na ndio maana mwaka uliopita tulianzisha mazungumzo baina ya vizazi, hata kabla ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kupendekeza mazungumzo hayo,” alisema Makori.

Kamishna huyo alitoa mfano na kaunti ya Marsabit ambapo maswala mengi yamesuluhishwa kupitia mazungumzo.

“Hapa  Marsabit wakati mizozo inazuka,mazungumzo ya mara kwa mara yalisaidia kupatikana kwa suluhu,” alidokeza kamoshma huyo.

Hata hivyo ili kuhakikisha ufanisi kamili, Dkt. Makori alisema mazungumzo hayo yanapaswa kutekelezwa kuanzia viwango vya mashinani, yaongozwe na watu na yadumishe mkondo ufaao.

Mtaalam wa mawasiliano kaunti ya Marsabit Farida Mohamed.

Kwa upande wake mtaalam wa mawasiliano kaunti ya Marsabit Farida Mohamed, alisema ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana ni changamoto kuu, ambalo linapaswa kushughulikiwa.

“Changamoto tunazokumbana nazo, zimetufikisha mahali tulipo,” alisema Mohamed.

“Maandamano ya Gen Z yamedhihirisha kwamba vijana hapa nchini wanataka kusikiliza,” aliongeza Mohamed.

Waliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mazungumzo baina ya vizazi yaliyozinduliwa Leo Alhamisi katika kaunti ya Marsabit na Time ya Uwiano na Utangamano wa Taifa NCIC kwa ushirikiano na shirika la Utangazaji Nchini KBC.

Share This Article