Halmashauri Huru ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA), imeelezea wasiwasi kuhusu jinsi maafisa wa polisi walivyokabiliana na waandamamaji, wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa mwaka 2024.
Ripoti iliyotolewa na Halmashauri hiyo, ilidokeza kuwa Wakenya 65 walifariki, huku raia 342 na maafisa wa polisi 171 wakijeruhiwa kwenye maandamano hayo, ambapo pia mali ya umma na ya kibinafsi iliharibiwa.
Ripoti hiyo iliongeza kuwa visa 48 dhidi ya dhuluma za polisi vilitolewa na vingine 70 kuripotiwa kwa IPOA, wakati wa maandamano ya Juni 25, 2025.
“Wakati wa maandamano hayo, IPOA imegundua ukiukaji wa katiba, ikiwa ni pamoja na utumizi wa nguvu kupita kiasi na ukosefu wa kulinda usalama na haki za binadamu,” ilisema taarifa hiyo ya IPOA.
IPOA iliendelea kusema kuwa maafisa wa polisi waliotumwa kutuliza ghasia, walitumia mbinu zilizosababisha maafa, kinyume na sehemu ya 37 ya katiba ya Kenya.
Kuhusu waandamanaji, IPOA ilidokeza kuwa walianza maandamano yao kwa amani, kabla ya kuingiliwa na wahuni waliodaiwa walikuwa wakilinda mali ya kibinafsi.
Kulingana na IPOA, watu 1,126 walitiwa nguvuni 223 wakifikishwa mahakamani kote nchini.